Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi waahidi kuhakikisha usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake

Viongozi waahidi kuhakikisha usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ni vigumu kutimiza ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu bila kuwa na haki sawa na kamili kwa nusu ya idadi ya watu duniani, kisheria na katika vitendo, akipigia chepuo usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake.

Ban amesema hayo akihutubia viongozi wa dunia, ambao wamekutana leo asubuhi mjini New York kutoa ahadi za kuchukua hatua kuhakikisha usawa na kuwawezesha wanawake katika ajenda ya maendeleo endelevu, katika kikao kilichoandaliwa na kusimamiwa na rais wa Uchina, Xi Jinping.

Katibu Mkuu amesema wanawake wengi na wasichana wanaendelea kubaguliwa, kukumbana na ukatili, kunyimwa fursa sawa katika elimu na ajira, na kutengwa katika nyadhfa za uongozi na maamuzi.

Ban ametoa wito kwa viongozi watoe ahadi za kuchukua hatua za kuhakikisha usawa wa jinsia kote duniani.

“Tunahitaji sayari yenye hamsini kwa hamsini ifikapo mwaka 2030. Tuongeze juhudi kupigania usawa wa jinsia. Kama viongozi wa nchi na serikali, mna uwezo na wajibu wa kuhakikisha kuwa usawa wa jinsia ni, na inabaki kuwa suala la kipaumbele kitaifa.”

Ban amesema kufikia usawa wa jinsia kunamaanisha kushughulikia vizuizi vya kimfumo kama vile tofauti za mishahara, kutambua na kushughulikia mzigo wa ulezi bila malipo kwa wanawake, kutambua haki ya wanawake na wasichana kudhibiti afya yao ya uzazi, kutokomeza ukatili dhidi yao, na usawa katika kushiriki katika siasa na katika jitihada za kibinadamu, utatuzi wa mizozo na ujenzi wa amani.