Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malipo ya kidigitali yainua maisha ya raia Tanzania: Kikwete

Malipo ya kidigitali yainua maisha ya raia Tanzania: Kikwete

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ameeleza kwamba idadi ya watu wanaopata huduma za fedha na benki imeongezeka mara nne tangu mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 58 nchini Tanzania, benki nane nchini humo zikitoa huduma za akiba na mikopo sasa kupitia simu za kiganjani.

Amesema hayo akihutubia mkutano kuhushu malipo ya kidigitali uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, wakati wa mkutano wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs, akisisitiza umuhimu wa huduma za malipo ya aina hiyo katika kuinua watanzania kutoka umaskini.

Akihojiwa na Idhaa hii baada ya mkutano huo Rais Kikwete amesema malipo ya kidigitali kupitia simu za kiganjani ni nuru sasa kwa wakulima, wafanyabiashara na wengine wanaoishi kijijini.

(Sauti ya Rais Kikwete)

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo UNDP bado watu milioni 2.5 duniani hawapati huduma za benki kabisa, UNDP ikisema kwamba malipo ya kidigitali na matumizi ya simu za kiganjani yanaweza kuchangia pakubwa katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya 2030 na kufikia maendeleo jumuishi.