Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa Safaricom aonyesha uhusiano wa sekta binafsi na #SDGs

Mkuu wa Safaricom aonyesha uhusiano wa sekta binafsi na #SDGs

Mkuu wa kampuni ya Safaricom nchini Kenya Bob Collymore amesema wananchi na wanahisa wanapaswa kuwajibisha mashirika binafsi ili yajitahidi kuimarisha utendaji kazi wa uwe endelevu zaidi.

Bwana Collymore amesema hayo alipohojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano wa sekta binafsi uliofanyika leo mjini New york Marekani sanjari na mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, mkutano uliohusisha wakuu wa kampuni mbalimbali akiwemo Mark Zuckerberg wa Facebook na viongozi wa kiserikali Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Ametolea mfano wa Kenya ambako amesema Safaricom inatumia teknolojia za habari na mawasiliano kukuza uchumi na maendeleo.

« Ukiangalia nishati safi tumefanya kazi kwa ushirikiano na M-Kopa ili kuleta nishati endelevu kwa wakenya maskini zaidi. Kuna maeneo mengine zaidi, ambapo tunatumia teknolojia zetu kutimiza malengo hayo, mara nyingi hazileti faida lakini zina manufaa kijamii na kibiashara. »

Akihutubia mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema malengo ya maendeleo endelevu yanaweza kunufaisha sekta binafsi iwapo…

« Kampuni zinapaswa kufanya biashara kwa kuwajibika na halafu kutafuta fursa mpya. Kwa kifupi, hazipaswi kuongeza matatizo duniani kabla hazijajaribu kuyatatua. Tutasogoelea dunia tunayotaka iwapo kampuni zitachukua hatua kama vile kuheshimu haki za wafanyakazi, kutochafua ardhi, bahari na anga, na kupambana na ufisadi. »