Skip to main content

Tuondolewe vikwazo ili tufanikishe ajenda 2030: Mugabe

Tuondolewe vikwazo ili tufanikishe ajenda 2030: Mugabe

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema nchi  yake imejipanga sawa ili kuhakikisha inafanikisha utekeleza wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Akihutubia mkutano mahsusi baada ya kupitishwa kwa malengo hayo yajulikanayo pia kama ajenda 2030, Rais Mugabe amesema baada ya mashauriano ya wadau mbali mbali wamepitisha mpango mpya wa kitaifa unaoendana ajenda hiyo mpya.

Mpango huo uitwao ZIMASEET una misingi mikuu minne ambayo ni uhakika wa chakula na lishe, huduma za jamii na kutokomeza umaskini, miundombinu na huduma pamoja na uongezaji thamani bidhaa.

Hata hivyo Rais Mugabe amesema mafanikio ya utekelezaji wa mkakati huo yatakuwa na dosari iwapo vikwazo dhidi ya Zimbabwe vilivyowekwa kwa miaka 15 sasa havitaondolewa.

Ametaka kuondolewa kwa vikwazo hivyo bila masharti yoyote ili ajenda 2030 iweze kuleta mabadiliko stahili kwa wananchi wa Zimbawe.