Skip to main content

Polio yatokomezwa Nigeria: WHO

Polio yatokomezwa Nigeria: WHO

Ugonjwa wa Polio si tatizo tena nchini Nigeria, limesema Shirika la Afya Duniani(WHO) huku likitoa hadhari kuwa nchi hiyo isibweteke bali iendelee kuwa makini.

WHO imesema tangu mwezi Julai mwaka jana Nigeria haijaripoti kisa chochote cha Polio licha ya kwamba katika miaka ya karibuni nchi hiyo iliongoza kuwa na nusu ya visa vya polio ulimwenguni.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema jitihada kati ya sekta ya umma na binafsi duniani katika kutokomeza polio zimefanikisha harakati hizo.

Kupitia GPEI wafanyakazi 200,000 wa kujitolea walikwenda katika sehemu mbali mbali nchini Nigeria kutoa chanjo dhidi ya Polio kwa watoto milioni 45 wenye umri wa chini ya miaka 5.

Dkt. Chan amesema dhamira na juhudi ambazo zimeitoa Nigeria katika orodha ya nchi zenye Polio, ni lazima ziendelee, ili tufikie bara la Afrika lisiwe kabisa na Polio na kwamba ni lazima kusaidia Pakistan na Afghanistan kufikia pia hatua hiyo.