Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Bilioni 25 kuepusha wanawake, watoto na vijana dhidi ya magonjwa:Ban

Dola Bilioni 25 kuepusha wanawake, watoto na vijana dhidi ya magonjwa:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza ahadi ya dola Bilioni 25 zitakazotumika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuboresha afya ya wanawake, watoto na vijana barubaru.

Tangazo hilo limetolewa kufuatia uzinduzi wa mkakati wa kimataifa kwa afya ya wanawake, watoto na vijana barubaru jijini New York, Marekani kando mwa mkutano wa kupitishwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ban amesema mkakati huo utasaidia kujenga jamii zenye uwezo wa kukinga na kushughulikia magonjwa na kwamba ni ishara kuwa ubia wa kimataifa unaweza kuzaa matunda.

Ahadi hiyo ya Ban imekuja wakati wakuu wa serikali na taasisi binafsi wakitangaza ahadi zao za kuboresha afya za kundi hilo kupitia mradi wa Every Woman Every Child.

Mathalani nchini Kenya, kampuni za Safaricom, MSD, Philips, GlaxoSmithKline, Huawei shirikisho la afya nchini Kenya wametiliana saini mkataba mpya wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi PPP wa kuinua afya ya zaidi ya watu Milioni Tatu nukta Tano nchini humo wakiwemo wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana barubaru.