Skip to main content

Ajenda 2030 yahitaji ushirikiano zaidi ili kufanikisha: Ethiopia

Ajenda 2030 yahitaji ushirikiano zaidi ili kufanikisha: Ethiopia

Tunapoanza zama za maendeleo mapya endelevu, tunahitaji jitihada za pamoja zaidi siyo kwa sababu malengo ni mengi kuliko yale ya milenia bali ni kwa sababu yanagusa dunia nzima.

Ni kauli ya Wazir Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn aliyotoa wakati akihutubia mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kupitishwa kwa ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs siku ya Ijumaa.

Amesema malengo hayo bila shaka yameazimia kubadili mfumo wa ushirikiano wa kimaendeleo duniani na kwamba kushindwa kuyafanikisha katika ukanda mmoja kutakuwa na madhara katika ukanda mwingine.

Bwana Dessalegn amesema moja ya fundisho la kukwama kwa baadhi ya malengo ya milenia ni kutokuwepo kwa mbinu za utekelezaji lakini kwa SDGs tayari mipango ilishaandaliwa na hivyo ni lazima kuizingatia akitolea mfano makubaliano ya Addis Ababa kuhusu ufadhili kwa maendeleo.

Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia amesema kwa Afrika, kupitishwa kwa ajenda hiyo ni mwanzo wa nuru ya  kutokomeza umaskini na kuanza safari njema ya kuinua uchumi na fursa za ajira kwa watu wote hususan vijana.