Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko pamoja na Burundi, wakiukwaji wa haki sheria ichukue mkondo wake:Ban

Tuko pamoja na Burundi, wakiukwaji wa haki sheria ichukue mkondo wake:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Makamu wa pili wa Rais wa Burundi Joseph Butore ambapo wamejadili usaidizi ambao umoja huo unaweza kupatia nchi hiyo wakati huu ambapo jitihada za kikanda zinaendelea kumaliza hali iliyopo nchini humo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akitoa hakikisho la usaidizi wa Umoja huo katika kupatia suluhu changamoto zote zinazokabili Burundi hivi sasa.

Amemhakikisha Makamu huyo wa Rais kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuendelea kushirikiana na Burundi katika kuimarisha utulivu na maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo Ban ameeleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mzozo wa kisiasa nchini Burundi na matukio ya ghasia yenye ushawishi wa kisiasa.

Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu akiisihi serikali kuharakisha uchunguzi na mchakato wa kisheria dhidi ya watu wote wanaohusika na ukiukaji wa haki. Halikadhalika ametaka uwepo wa mashauriano jumuishi ya kisiasa bila kuchelewa.