Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda ya maendeleo endelevu ama SDGs yapitishwa

Ajenda ya maendeleo endelevu ama SDGs yapitishwa

Ajenda ya maendeleo endelevu au SDGs imepitishwa rasmi leo na nchi wanachama 193 ya Umoja wa Mataifa, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema hatua kutoka kwa kila mtu duniani inahitajika.

Amesema utashi wa kisiasa unahitajika, na pia ubia wa kimataifa ili kuhakikisha utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030, ambayo inataka kuhakikisha hakuna mtu atakayeachwa nyuma.

"Ili kuimarika, tunapaswa kubadilika. Ajenda ya mwaka 2030 inatulazimisha kuangalia mbali na mipaka ya kitafia na upendeleo wa muda mfupi, na kuchukua hatua pamoja kwa ajili ya muda mrefu. Hatuwezi tena kufikiria na kufanyakazi bila ushirikiano."

Halikadhalika Katibu Mkuu amesema taasisi zinapaswa kuimarika ili kutekeleza SDGs, akisema kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia nchi wanachama katika jitihada hizo.

Aidha amezingatia umuhimu wa kuafikia kuhusu mabadiliko ya tabianchi ifikapo mkutano wa COP21 utakaofanyika mjini Paris Ufaransa.

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa haki na mshindi wa Tuzo ya Nobel Malala Yousafzai ametoa wito kwa viongozi wa dunia akisimama pamoja na watoto 193 kutoka kila nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

"Wapendwa viongozi wa dunia, toeni ahadi kwa kila mtoto, toeni ahadi kwamba kila mtoto atapata haki ya elimu ya msingi na sekondari ikiwa bure, salama na bora. Huu ndio uwekezaji wa kweli ambao dunia inahitaji na ambao viongozi wa dunia wanapaswa kufanya."