Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Yoweri Museveni wa Uganda afungua rasmi mkutano wa SDGs

Rais Yoweri Museveni wa Uganda afungua rasmi mkutano wa SDGs

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema wakati mpya unaanza sasa katika jitihada za kutokomeza umaskini na kulinda sayari ya dunia.

Museveni ambaye ni mwenyekiti mwenza wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu malengo ya maendeleo endelevu amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa cha kupitisha malengo hayo ambapo amepongeza jitihada za viongozi wa kimataifa katika uundaji wa malengo hayo.

“Pamoja tunatuma ujumbe wenye nguvu kwa watu katika kila kijiji, kila mji, kila taifa duniani kote kwamba tunajituma kuchukua hatua thabiti ili kubadilisha maisha yao ile yawe bora “.

Aidha amemulika mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa malengo ya milenia MDGs akichukua mfano wa Uganda, ambapo kiwango cha umaskini kimepungua kutoka kwa asilimia 56 mwaka 2000 hadi 19 tu mwaka huu.

Rais Museveni amesema cha msingi sasa ni utekelezaji wa SDGs akisisitiza umuhimu za kuyaunganisha kwenye sera za kitaifa na kuyapatia ufadhili wa kutosha.

Hata hivyo amezingatia mahitaji ya nchi zinazoendelea katika maswala ya ufadhili, pamoja na uwakilishi katika vyombo vya Umoja wa Mataifa.