Skip to main content

Papa Francis ahutubia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, New York

Papa Francis ahutubia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, New York

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis amewasili katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo katika tukio la kwanza, amezungumza na wafanyakazi wa umoja huo.

Akimkaribisha Papa Francis kuwahutubia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema ingawa ni yeye ndiye anayeonekana zaidi, ni wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ndio wanaoubeba umoja huo,

“Ni wao wanaofanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya amani, maendeleo na haki za binadamu kote duniani. Ahsante kupata muda wa kukutana nao, kwani ni wao ndio moyo na roho ya kazi yetu. Bila kujali Imani, tunahamasishwa na unyenyekevu na utu wako, na wito wako wa kuchukua hatua kwa ajili ya haki ya kijamii, mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha maisha yenye utu kwa watu wote. Gracias. Merci. Shukran. Xie xie. Spasibo.”

Akiwahutubia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, Papa Francis amesema, ingawa kazi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa haionekani katika vyombo vya habari kila siku, lakini juhudi zao za kila siku ni muhimu mno..

Juhudi zenu za kila siku zinawezesha mikakati mingi ya kidiplomasia, kitamaduni, kiuchumi na kisiasa ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni muhimu sana katika kutimiza matumaini na matarajio ya watu wote, ambao ni familia ya ubinadamu. Ahsanteni kwa yote mnayofanya.”

Papa amesema kazi ya kimyakimya na bidii, haichangii tu kuboresha Umoja wa Mataifa, lakini pia ina umuhimu mkubwa kwao binafsi, kwani jinsi watu wanavyotenda kazi inaonyesha utu na sifa zao kama watu.

“Wengi wenu mmekuja kwenye mji huu kutoka nchi duniani kote. Kwa hiyo, nyinyi ni wawakilishi wa watu ambao Umoja huu unawakilisha na kuhudumia.”

Baada ya kukutana na kuzungumza na wafanyakazi Papa Francis ameweka shada la maua kukumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakiwa wanahudumu kwa ajili ya amani duniani.