Harakati za mpito zaanza upya Burkina: Mjumbe wa Umoja wa Mataifa
Mchakato wa mpito umeanza upya nchini Burkina Faso, amesema Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi, Mohammed Ibn Chambas, akieleza kufuraishwa na kurejeshwa madarakani kwa Rais wa mpito Michel Kafando jumatano hii.
Akiongea leo na Redio ya Umoja wa Mataifa, Bwana Chambas amesema kwamba baraza la mawaziri litakutana ijumaa hii ili kuafikia kuhusu ratiba mpya ya uchaguzi na kuendelea kwa mazungumzo.
“ Tumefurahi kwamba rais Kafando amerudi ofisini sasa, na kwamba serikali ya mpito imerejeshwa. Tunapendekeza mazungumzo baina ya wadau wa Burkina, ili kuhakikisha mazingira yenye amani hadi mwisho wa wakati wa mpito ili kufanikisha uchaguzi jumuishi na wa kuaminika. ”
Aidha amesema Umoja wa Mataifa umejiandaa kutuma timu ya wachunguzi na watalaam wa haki za binadamu ili kufuatilia vitendo vya ukatili dhidi ya raia.