Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika inapaswa kuwa tayari kukabili ukuaji wa miji: Ban Ki-moon

Afrika inapaswa kuwa tayari kukabili ukuaji wa miji: Ban Ki-moon

Bara la Afrika ndio sehemu ya dunia ambapo miji inakuwa kwa kasi zaidi, ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika mjadala maalum uliofanyika leo mjini New York Marekani, kuhusu Ajenda ya ukuaji wa miji barani Afrika.

Katika hotuba yake, Bwana Ban amesema ukidhibitiwa na kuongozwa vizuri, ukuaji wa miji unaweza kuwa nyenzo ya maendeleo endelevu, akieleza kwamba lengo namba 11 la malengo ya maendeleo endelevu au SDGs, linalenga kusaidia ukuaji wa miji kuwa jumuishi, salama na endelevu, kwa kuhakikisha nguzo tatu za maendeleo endelevu zinaheshimiwa zikiwa ni uchumi, jamii na mazingira.

Amesema Afrika inapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto hiyo.

“ Mabadiliko ya kimkakati yanahitajika. Sera za kitaifa za miji ni nyenzo nzuri ya kuongoza mjadala, kuleta maelewano na kuunda mkakati. Katika ngazi ya mitaa, ni lazima kulenga harakati zinazoheshimu mahitaji ya maeneo hayo, jamii na mazingira. Ukiongozwa vizuri, ukuaji wa miji unaweza kuleta manufaa mbali na mipaka ya miji hadi vijijini.”