UNAIDS yatoa wito kwa serikali na sekta ya dawa ziendeleze ahadi ya dawa nafuu

UNAIDS yatoa wito kwa serikali na sekta ya dawa ziendeleze ahadi ya dawa nafuu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Ukimwi, UNAIDS, limetoa wito kwa serikali na sekta ya kuunda dawa zihakikishe kuwa dawa zinaendelea kupatikana kwa watu wote, wakati viongozi wakikutana jijini New York kuridhia malengo ya maendeleo endelevu, yakiwemo malengo madogo kabambe yanayohusu afya ya umma.

Kuongezeka kasi kwa gharama ya baadhi ya dawa inaongeza wasiwasi kuhusu upatikanaji endelevu wa dawa hizo kwa wagonjwa, pamoja na athari nyingine kwa sekta ya afya ya umma.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS,  Michel Sidibé, amesema serikali na sekta binafsi zina wajibu wa kuhakikisha dawa zinaendelea kupatikana kwa kila mtu, akiongeza kuwa jitihada dhidi ya Ukimwi zimethibitisha kuwa upatikanaji wa dawa stahiki zenye gharama nafuu unaweza kubadili mwelekeo wa mlipuko wa ugonjwa.

Zaidi ya watu milioni 15 sasa wanapata dawa za kuokoa maisha za ARV, ikilinganishwa na idadi chini ya 700,000 mwaka 2000.

UNAIDS iliweka lengo jipya la matibabu la 90-90-90 hadi mwaka 2020, ikilenga kutokomeza ukimwi kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.