Ashish Thakkar aeleza matumaini yake kuhusu biashara barani Afrika
Wakati wa Afrika ni sasa! Hii ni kauli ya Ashish Thakkar, mfanya biashara mwenye uraia wa Uganda na Rwanda na mwenye asili ya India, ambaye ni miongoni mwa wawekezaji tajiri zaidi barani Afrika, leo akizindua kitabu chake kiitwacho "The Lion Awakes" yaani simba aamka.
Bwana Thakkar ambaye pia ni mwenyekiti wa Kikao cha wafanyabiashara kwenye wakfu wa Umoja wa Mataifa, UN Foundation, amesema kwamba fursa za uwekezaji ni nyingi barani Afrika na tayari nchi nyingi zinataka kulingana na nchi zingine barani Asia katika ufanisi wa kiuchumi, mfano Rwanda.
Akiongea na idhaa hii baada ya uzinduzi huo, Bwana Thakkar amesema changamoto kubwa bado ni ukosefu wa uzalishaji wa nishati barani humo, na pia swala la utawala bora.
Hatimaye ametoa ushauri kwa vijana wa ukanda wa Afrika Mashariki ambao wanatafuta ajira au fursa ya kufanya biashara.
"Chapa kazi, kuwa na fikra kubwa… Fikiria mno, uwe na ndoto, lakini uanze na kitu kidogo, uwe na mtazamo wa mbali. Uwe na maadili na zingatia masharti, lakini uanze na kitu kidogo na usiwe na ubinafsi. Chapa kazi, utashindwa mara nyingi lakini uwe na bidii, uanze tena."