Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na mapigano na uharibifu Yemen

Ban asikitishwa na mapigano na uharibifu Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na mapigano na mashambulizi ya angani ambayo yamesababisha uharibifu zaidi katika miji ya Yemen, na kuongezeka hata zaidi kwa idadi ya wahanga wa kiraia katika siku chache zilizopita.

Akikumbusha kuwa pande zote katika mzozo huo zina wajibu wa kuchukua tahadhari zote stahiki kuzuia vifo vya raia na uharibfu wa mali za raia, Katibu Mkuu amekariri haja ya uwajibishaji kwa ukiukaji mbaya wa sheria ya kimataifa ambao huenda umefanywa katika mzozo huo.

Aidha, Katibu Mkuu amekaribisha kuachiliwa kwa raia watatu wa Saudia, wawili Wamarekani na mmoja Mwingereza, ambako kulifanywa na WaHouthi mnamo Septemba 20, 2015, akitaja kitendo hicho kama hatua madhubuti katika juhudi za kupunguza utata katika ukanda wa Mashariki ya Kati na kufungua njia ya kupatia suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Yemen.