Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kuboresha mchakato wa uchaguzi wa Katibu Mkuu UM zaendelea

Harakati za kuboresha mchakato wa uchaguzi wa Katibu Mkuu UM zaendelea

Tutahakikisha mchakato wa kumpata Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa unakuwa wa wazi na shirikishi tofauti kabisa na ilivyokuwa tangu mwaka 1945.

Ni kauli ya William Pace, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Global Policy aliyotoa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuhusu mchakato wa kupatikana kwa kiongozi huyo wakati huu ambapo Katibu Mkuu wa sasa anahitimisha awamu yake mwakani.

Bwana Pace amesema ..

(Sauti ya Pace)

“Hapo awali ilikuwa vigumu sana hata kuwafahamu wagombea nafasi hiyo, sifa zao, dira zao na ahadi wanazolazimishwa kutoa ili wasipigiwe kura turufu na nchi wanachama. Ni matarajio yetu kuwa mchakato huo mzima utabadilika kabisa sasa kufuatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, uteuzi wa wajumbe kwenye baraza na tamko la Uingereza kuwa inataka kubadili mchakato huo.”

Naye Nathalie Samarasinghe, Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha Umoja wa Mataifa nchini Uingereza amesema lengo ni kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katibu Mkuu tofauti na awali..

(Sauti ya Nathalie)

 "Kwa kuwa na mchakato huu wa wazi tutainua ubora wa mchakato mzima, na hii ni njia ya kuboresha mchakato huu kuanzia sasa na kuendelea.”

Harakati za kuboresha mchakato huu zimeshika kasi baada ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 11 mwezi huu wa Septemba kupitisha azimio namba 69/321 lenye lengo la kuweka wazi zaidi mfumo wa uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.