Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Libya: Tumekamilisha kazi asema mwakilishi wa Ban Ki-moon

Libya: Tumekamilisha kazi asema mwakilishi wa Ban Ki-moon

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wka Libya, Bernadino Leon, amesema utaratibu wa mazungumzo ya amani umekamilishwa kazi imebakia kwa pande husika kwenye mzozo huo. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Bwana Leon amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Skhirat, nchini Morrocco, baada ya awamu nyingine ya mazungumzo baina ya pande za mzozo za Libya iliyofikia rasimu ya mwisho ya nyaraka ya makubaliano, akisema kwamba kazi ya Umoja wa Mataifa umekwisha na mradi huu ndio suluhu kwa Libya.

“Habari njema kwa nchi hii na kwa jamii ya kimataifa ni kwamba leo kuna uwezekano wa wazi kwamba machafuko yanaweza kuisha, na umoja ambao utawawezesha Libya kurejelea nchi nzuri na tajiri na mfano mzuri wa suluhu ya kisiasa kupitia mazungumzo wala si kupitia ghasia na vita.”

Bwana Leon amesema hatua nyingine ni wawakilishi wa pande za mzozo wachague watakaoshiriki kwenye serikali na hatimaye waiweke saini rasmi nyaraka hiyo ya makubaliano kabla ya ukomo wa wakati wa mpito tarehe 20, Oktoba.

Aidha amesema mkutano maalum wa ngazi ya juu unatakiwa kufanywa mwisho mwa mwezi huu mjini New York, Marekani.