Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majira ya baridi kali kuongeza machungu kwa wakimbizi Ulaya: Lykketoft

Majira ya baridi kali kuongeza machungu kwa wakimbizi Ulaya: Lykketoft

Rais wa Baraza Kuu Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani na kusema kuwa zahma inayokumba wakimbizi wanaosaka hifadhi barani Ulaya itakuwa kubwa zaidi wakati huu ambapo msimu wa baridi kali unakaribia.

Amesema hali hiyo ya sasa ni janga kubwa dunia kuwahi kushuhudia tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia na pengine hali ni mbaya zaidi kuliko inayoelezwa kupitia vyombo vya habari kwa hivyo..

(Sauti ya Lykketoft)

“Nchi tajiri, kama nilivyosema zinatakiwa ziendelee kukaribisha wakimbizi zaidi au zitoe fedha za kuwasaidia na bora zaidi yote mawili. Hakuna fursa ya kukataa yote hayo mawili. Si kosa kusaka ukimbizi au kusaka hifadhi. Mustakhbali wa mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto uko hatarini. Tunapaswa kuhakikisha maamuzi yetu yanatekelezeka na yenye mwelekeo na tunasaka kupata majibu endelevu."

Rais huyo wa Baraza Kuu akasema anasubiria kwa hamu kuwa na mazungumzo na kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Pope Francis baadaye wiki hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo waandishi wa habari walimuuliza ni jambo gani hasa atapende kuzungumza naye?

(Sauti ya Lykketoft)

“Bila shaka nataka kumshukuru kwa jinsi anavyotilia mkazo mahsusi kwenye suala la mahitaji ya kibinadamu katika mazingira ya sasa. Na nina matumaini na uhakika kuwa ataendelea kutumia uongozi wake kushawishi wakuu wa nchi na serikali kuchukua hatua na wachukue hatua sasa.”