Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaya sasa inalipa gharama mzozo wa Syria: Pinheiro

Ulaya sasa inalipa gharama mzozo wa Syria: Pinheiro

Mwenyekiti wa Kamisheni ya uchunguzi kuhusu Syria, Paulo Pinheiro, amelieleza Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba taifa la Syria limefilisika kutokana na zaidi ya miaka minne ya vita huku jamii ya kimataifa ikishuhudia.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza hilo mjini Geneva, Uswisi, Bwana Pinheiro amesema vita hivyo vikali vimeharibu umoja wa nchi hiyo uliokuwa umejengwa katika misingi ya jamii zenye mila na dini tofauti, huku majengo ya kihistoria yakibomolewa na kundi la kigaidi la ISIS.

Ameongeza kwamba Ulaya sasa imeanza kulipa gharama ya vita hivyo, wakimbizi wakikimbilia bara hilo kwa wengi, kwa sababu wanalengwa moja kwa moja na pande za mzozo.

Aidha bwana Pinheiro amesikitishwa na kuona kwamba bado silaha na fedha zinapelekwa nchini humo akisema hilo linapaswa kusitishwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Syria kwenye mjadala huo amesema ripoti hiyo haikuangalia jinsi nchi mbalimbali zikiwemo Uturuki, Saudi Arabia, Uingereza na Marekani zinafadhili waasi, ambao wanatesa raia.