Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hungary zingatia haki za watoto wakimbizi: UNICEF

Hungary zingatia haki za watoto wakimbizi: UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, linawasiliana na mwakilishi wa kudumu wa Hungary kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kujadili jinsi ya kulinda watoto wakimbizi na wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Taarifa ya UNICEF inasema mazungumzo hayo yanaangalia jinsi watoto wakimbizi na wahamiaji wanaweza kulindwa kwa mujibu wa ahadi za nchi hiyo za kutekeleza mkataba wa haki za mtoto, CRC.

Mkataba huo unataka serikali kuchukua hatua stahiki kulinda watoto ambao ni wakimbizi sambamba na wale wanaosaka hifadhi.

Mazungumzo yanafanyika wakati tayari UNICEF imeanza kusaidia Hungary kufuatia ghasia za mpakani mwa Hungary na Serbia ambako watoto walijikuta katikati ya ghasia huku kukiwa na ripoti kuwa Hungary imepitisha sheria mpya inayoweza kusababisha watoto wanaoingia nchini humo kushikiliwa, kufunguliwa mashtaka na kutenganishwa na wazazi wao.

Msaada huo ni pamoja na kuwapatia ushauri wa kisaikolojia watoto na kubaini na kusaidia watoto wanaosafiri peke yao.