Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Mkuu wa UNRWA Pierre Krähenbühl azuru Syria

Kamishna Mkuu wa UNRWA Pierre Krähenbühl azuru Syria

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, Pierre Krähenbühl, hapo jana amehitimisha ziara yake ya siku tatu nchini Syria, ambako alikutana na wakimbizi wa Kipalestina, wafanyakazi wa UNRWA na maafisa wa serikali.

Akiwa mijini Homs na Damascus, Bw. Krähenbühl alielezea shukrani na mshikamano wake kwa kazi ya ujasiri na kujitoa ya wafanyakazi wa UNRWA, ambao hufanya kazi katika mazingira magumu, wakikabiliwa na hatari kila siku wanapofikisha huduma muhimu kwa wakimbizi wa Palestina, ambao wamelazimika kuhama kutokana na mgogoro.

Akikutana na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali, Kamishna huyo mkuu amesisitiza umuhimu wa kuwezesha ufikishaji misaada ya kibinadamu kwa kambi zote za wakimbizi wa Palestina na jamii, ikiwemo Yarmouk na maeneo jirani, na Khan Eshieh, ambako wakimbizi wana mahitaji makubwa, yakiwemo kuendelea kuishi.