Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi Nigeria yasambaratisha watoto zaidi ya Milioni 1.4

Mashambulizi Nigeria yasambaratisha watoto zaidi ya Milioni 1.4

Nchini Nigeria kasi ya ongezeko la mashambulizi kutoka wka kikundi cha Boko Haram kimesababisha watoto zaidi ya Milioni Moja na Laki Nne kukimbia makwao nusu yao wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema kiwango hicho ni kikubwa na katika miezi mitano pekee watoto Laki Tano walikimbia jambo linalosababisha kukatisha maisha ya utoto wao.

UNICEF imesema hali inatia hofu kushuhudia watoto na wanawake wakiendelea kuuawa, kutekwa nyara na kulazimishwa kubeba mabomu na hadi sasa wameweza kutoa huduma muhimu za kiafya kama vile chanjo lakini wanahitaji fedha zaidi kwani  wamepokea asilimia 32 tu ya dola zaidi ya Milioni 50 wanazohitaji kuimarisha usaidizi.

Christopher Boulierac ni msemaji wa UNICEF Geneva.

(Sauti ya Christophe)

"Kuna watu wengi zaidi wenye mahitaji na ufadhili ni mdogo. Ni vigumu kukidhi mahitaji muhimu, na uwezo wetu wa kuwasilisha mahitaji muhimu uko mashakani na huu ni wakati muafaka wa vitendo. Msimu  huu wa mwambo ukifikia ukomo watu waliofurushwa makwao na wale wanaowahifadhi wanafikia ukomo wa uwezo wa kujihudumia na akiba ya chakula inakwisha."

Amesema idadi ya wakimbizi inaongezeka na bila fedha za kutosha ina maana watashindwa kuwapatia huduma za muhimu kama vile afya, elimu na maji safi na salama.