Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa serikali na sekta binafsi waweza fanikisha ufadhili wa SDG

Ubia wa serikali na sekta binafsi waweza fanikisha ufadhili wa SDG

Wakati malengo ya maendeleo endelevu, SDG au ajenda 2030 ikitarajiwa kuridhiwa na wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wiki ijayo mjini New York, Marekani bado inelezwa kuwa kisichoeleweka ni  jinsi ya kupata mabilioni ya pesa ya kugharamia malengo hayo.

Njia mojawapo inayoangaziwa ni kuhamasisha uwekezaji wa sekta ya kibinafsi katika kujenga miundombinu, barabara, daraja na mabwawa, ambayo yatahakikisha kuwa nchi zinaweza kukua bila kufilisisha serikali.

Ni kwa mantiki hiyo tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi barani Ulaya, UNECE imeandaa maonyesho huko Geneva, Uswisi kudhirisha jinsi ubia kati ya serikali na sekta binafsi, PPP unaweza kufanikisha malengo hayo.

Imetolea mfano mradi wa aina hiyo huko Belarus wa ujenzi wa barabara kubwa ya kuunganisha nchi za Muungano wa Ulaya na Asia ukiwa na  thamani ya dola Milioni 350, mradi ambao unaelezwa utainua uchumi wa nchi husika.

Katibu Mtendaji wa UNECE  Christian Friis Bach akizungumza kwenye maonyesho hayo amesema serikali haziwezi kutekeleza malengo peke yake, badala sekta binafsi lazima ijumuishwe katika mfumo ambao utakuwa na manufaa kwa lengo la kulinda wawekezaji na walipa kodi.