Juhudi zaidi zahitajika kushughulikia mizizi ya kinachowafurusha watu makwao- O’Brien

Juhudi zaidi zahitajika kushughulikia mizizi ya kinachowafurusha watu makwao- O’Brien

Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, amesema leo kuwa Hatma ya Wasyria wanaojaribu kuingia Ulaya imeonyesha kuwa madhara ya mzozo wa Syria siyo tu kwa taifa au ukanda, bali ni ya kimataifa.

Akisema kuwa mgogoro wa Syria umeibua moja ya mmiminiko mkubwa zaidi wa wakimbizi tangu vita vikuu vya pili vya dunia, Mkuu huyo wa OCHA amesema wakimbizi hao wanakimbia machafuko na ukatili, na wana haki ya kuomba hifadhi bila aina yoyote ya ubaguzi.

Bwana O’Brien ambaye amekuwa akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo, amesema ni wajibu wa jamii ya kimataifa kuzisaidia nchi jirani za Syria kuubeba mzigo wa wakimbizi hao.

Aidha, Bwana O’Brien amemulika vyanzo vya mzozo huo wa wakimbizi

“Wakati huohuo, juhudi zaidi zinapaswa kuelekezwa katika kushughulikia mizizi ya kinachowalazimu watu kukimbia makwao na kutafuta hifadhi salama ng’ambo, na kushughulikia hali ya ‘kimbia au ufe’ ambayo ni kawaida kwetu sote tunapokabiliwa na maafa au hatari kwa maisha yetu. Kwa Syria, inapaswa ifahamike dhahiri kwa wote kuwa hii inamaanisha kuwa na suluhu la kisiasa litakaloumaliza mzozo huu.”

Halikadhalika Bwana O’Brien amesema kuwalenga raia na miundombinu ya kiraia kwa kukusudia kunaendelea nchini Syria mara kwa mara, akitaka pande husika zikome kufanya hivyo na kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na ya kibinadamu.