Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nishati inaunganisha ukuaji wa uchumi, usawa wa kijamii na ubora wa mazingira- Ban

Nishati inaunganisha ukuaji wa uchumi, usawa wa kijamii na ubora wa mazingira- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema leo kuwa nishati ndio uzi muhimu unaounganisha ukuaji wa uchumi, usawa katika jamii na ubora wa mazingira. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katibu Mkuu amesema hayo wakati wa mkutano kuhusu Nishati Endelevu kwa Wote, akisifu kujumuishwa kwa lengo nambari saba kuhusu nishati katika malengo ya maendeleo endelevu.

Ban amesema mkakati wa nishati endelevu kwa wote utaunga mkono lengo hilo, kwani unatoa mwongozo wa kulitekeleza.

“Tumeweka msingi wa kuunga mkono utekelezaji wa lengo namba saba la SDG. Lakini tunaweza, na ni lazima tujitahidi zaidi. Ili kutimiza uwezo wa nishati endelevu kwa wote kikamilifu, tunahitaji mkakati wa muda mrefu wa kitaasisi.”

Akiongea wakati wa mkutano huo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji wa mkakati wa Nishati Endelevu kwa Wote anayeondoka, Kandeh Yumkella, amesema kufanikiwa kwa malengo mengine ya maendeleo endelevu kunategemea nishati endelevu kwa wote

“Bila upatikanaji wa nishati endelevu yenye gharama nafuu na inayotegemewa, hakuna lengo jingine la maendeleo endelevu litakalotimizwa, na bila shaka, hatutatua tatizo la mabadiliko ya tabianchi.”

Wakati huo huo, Ban ametangaza kuteuliwa kwa Rachel Kyte kutoka Benki ya Dunia kama Mkuu mpya wa mkatati wa Nishati Endelevu Kwa Wote."