Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utunzaji wa tabaka la ozoni ni mfano wa kuigwa: Ban

Utunzaji wa tabaka la ozoni ni mfano wa kuigwa: Ban

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya utunzaji wa tabaka la ozoni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amesema jinsi dunia ilivyoweza kudhibiti tundu lililokuwepo kwenye tabaka hilo kwa kupunguza matumizi ya gesi aina ya CFCs ni mafanikio makubwa yanayopaswa kuigwa wakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Kwenye ujumbe wake kwa siku hii, Bwana Ban amesema wakazi wa dunia wanapaswa kutunza tabianchi jinsi ambavyo walitunza tabaka la ozoni, akisema mikataba iliyosainiwa mwaka 1985 mjini Vienna na Montreal mwaka 1987 imewezesha jamii ya kimataifa kuchukua hatua ili kusitisha uharibifu wa tabaka hilo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP, visa milioni 2 vya saratani ya ngozi vinazuiliwa kila mwaka kutokana na juhudi hizo na kwamba tundu la tabaka la ozoni linatarajiwa kuziba kabisa ifikapo 2050, jitihada zikiendelea.

Aidha Katibu Mkuu ameonya kwamba gesi aina za HFC zinazotumiwa badala ya CFCs zinazalisha kiasi kikubwa cha gesi chafuzi na hivyo kusababisha ongezeko la  joto duniani, akisema hatua inayopaswa kuchukuliwa sasa ni kudhibiti gesi hizo, wakati ambapo nchi wanachama za Umoja wa Mataifa zinatarajia kuafikia kuhusu hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi mjini Paris Ufaransa mwezi Disemba mwaka huu.