Skip to main content

Baraza la Haki za Binadamu lajadili kujumuishwa suala la jinsia katika kazi yake

Baraza la Haki za Binadamu lajadili kujumuishwa suala la jinsia katika kazi yake

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo Jumanne limefanya mkutano wake wa kila mwaka kuhusu kujumuisha suala la jinsia katika kazi yake yote na katika mikakati yake, kwa kumulika usawa wa jinsia.

Rais wa Baraza hilo, Joachim Rücker, amesema wanawake wanawakilisha watu bilioni 3.5 duniani, au zaidi ya asilimia 50 ya idadi nzima ya watu duniani, lakini katika nchi nyingi, wanakabiliwa na vizuizi vingi katika kushiriki ipasavyo katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema uwakilishi sawa wa wanawake na wanaume katika ngazi zote za kufanya uamuzi, ajira, na elimu, ni ishara muhimu ya kupiga hatua za kufikia usawa wa jinsia.

Ameongeza kuwa ni suala la msingi la haki, na kwamba wanawake na wanaume wanatakiwa waweze kushiriki katika nyanja zote za maisha kwa usawa.