Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi Mwema wa UNICEF, David Beckham ataka viongozi watokomeze ukatili dhidi ya watoto

Balozi Mwema wa UNICEF, David Beckham ataka viongozi watokomeze ukatili dhidi ya watoto

Balozi Mwema wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, David Bekham, anapigia chepuo barua iliyoandikwa na manusura kumi na wanane wa ukatili dhidi ya watoto, ikitoa wito kwa viongozi duniani kutokomeza unyanyasaji wa watoto ulioenea, na ambao unaathiri mamilioni ya watoto kote duniani. Taarifa kamili na Joshua Mmali

(Taarifa ya Joshua)

Mmoja wa watoto waliosaini barua hiyo ni mvulana mwenye umri wa miaka 16 kutoka Cambodia, ambako Beckham alizuru mapema mwaka huu.

Beckham amesema aliposafiri kwenda Cambodia na UNICEF mapema mwaka huu, alipata kukaa na watoto na vijana ambao wamekumbana na ukatili mbaya na unyanyasaji, aghalabu mikononi mwa watu waliopaswa kuwalinda.

“ Nimekutana na watoto wengi mno walioathirikika na ukatili na mateso. Watoto waliotelekezwa, wanaoishi barabarani, wanaolazimishwa kufanya kazi. Watoto walio hatarini. Hakuna mtoto anayepaswa kuanza maisha yake hivyo. Viongozi wa dunia wanapaswa kuchukua hatua sasa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto. Tusipochukua hatua sasa, nani atafanya hivyo?”

Wiki ijayo, Beckham ataungana na Katibu Mkuu Ban Ki-moon na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake kuzindua malengo ya maendeleo endelevu, na kutoa wito kwa viongozi watoe kipaumbele kwa watoto wanapofanya uamuzi na uwekezaji katika miaka 15 ijayo.