Skip to main content

UM kuridhia malengo 17 ya maendeleo endelevu, SDGs

UM kuridhia malengo 17 ya maendeleo endelevu, SDGs

Mwisho wa mwezi huu wa Septemba viongozi 193 wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa watakutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kwa ajili ya kuamua rasmi kuhusu ajenda 2030.

Ajenda hiyo yenye malengo 17 ya maendeleo endelevu yanalenga pamoja na mambo mengine kutokomeza umaskini uliokithiri, kupambana na tofauti na ukosefu wa haki na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa nini mwaka huu?

Malengo ya Maendeleo ya Milenia au MDGs yameundwa mwaka 2000 yakilenga kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Kinachohojiwa ni kwa nini hatua hizi zitimizwe nusu? Ni lazima zikamilishwe hivyo mwaka huu wa 2015, mpango mwingine wa miaka 15 umeundwa kwa ajili ya kutekeleza malengo hayo ya maendeleo endelevu au SDGs ifikapo mwaka 2030.

Maendeleo endelevu ni kitu gani?

Maendeleo endelevu yanalenga kutimiza mahitaji ya wakati wa sasa bila kuathiri mahitaji ya vizazi vijavyo. Inamaanisha kuendelea kukuza uchumi bila kuendelea kuchafua mazingira na kuathiri jamii na vizazi vijavyo.

Mbona malengo ni mengi?

Changamoto zinazokumba dunia ya leo ni nyingi zaidi na kwa hiyo viongozi wameafikia malengo makubwa 17 yenye malengo madogo madogo 169, yakiwa ni matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima, yakishirikisha jamii na wadau mbali mbali, tofauti na utaratibu uliofanyika wakati wa MDGs.

Nani atakatekeleza malengo?

Kinyume na MDGs, SDGs zinapaswa kutekeleza na kila nchi iwe imeendelea au inaendelea.

Nchi 193 zitawajibika wanachama wa Umoja wa Mataifa, zikifuatiliwa na Umoja wa Mataifa, pamoja na mashirika ya kimataifa na raia kwa ujumla, Umoja wa Mataifa ukitoa wito kwa ushirikiano wa wote katika mpango huo.