Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 69 cha Baraza Kuu chahitimishwa kwa sifa kemkem

Kikao cha 69 cha Baraza Kuu chahitimishwa kwa sifa kemkem

Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kimehitmishwa leo, huku Baraza hilo likipongezwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon kwa mafanikio yake katika kikao hicho.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kufunga kikao hicho, Katibu Mkuu amesema wakati muhimu zaidi katika kikao hicho cha 69 ulikuwa bila shaka kupitishwa kwa ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

“Ajenda hiyo mpya imetokana na mshikamano unaohamasisha. Kutunga malengo makuu 17 na malengo madogomadogo 169 hakukutimia kwa siku moja. Ajenda ya 2030 ni ishara ya ahadi ya Umoja huu kupunguza taabu sasa, huku ikiweka mustakhbali bora kwa vizazi vijavyo. Napongeza tena nchi wanachama kwa kuinyakua fursa hii ya kihistoria kwa mtazamo wa kujenga na kujitoa.

Akilihutubia Baraza hilo kwa mara ya mwisho kama rais wake, rais anayeondoka, Sam Kutesa, amekariri ujumbe huo wa kikao cha 69 kutoa fursa ya kihistoria ya kuubadili ulimwengu ili uwe bora zaidi.

Bwana Kutesa ametaja makubaliano kuhusu ajenda ya maendeleo ya 2030 kuwa moja ya matukio makuu zaidi ya kikao cha 69, kwani nchi wanachama ziliweka juhudi kubwa katika kubuni na kutunga mkakati wa maendeleo ambao ni jumuishi na wa kuleta mabadiliko.

“Nashukuru na kuwapongeza wote waliohusika katika mchakato wa mazungumzo kwa kujitoa kwao thabiti katika kuunda ajenda kabambe. Ningependa hasa kuwashukuru Balozi David Donoghue, Mwakilishi wa Kudumu wa Ireland na Balozi Macharia Kamau, Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwa juhudi zao yakinifu katika kuongoza mashauriano hadi tamati yenye ufanisi.

Bwana Kutesa amesema ajenda hiyo itaongoza juhudi za maendeleo kwa miaka 15 ijayo, ikizingatia mahitaji ya watu wote duniani, wakiwemo vijana, wanawake, walemavu na walio hatarini zaidi, na itagusa moja kwa moja maisha ya watu sasa na katika vizazi vijavyo.