Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulitimiza mengi, asema Kutesa akihitimisha Urais wa Baraza Kuu

Tulitimiza mengi, asema Kutesa akihitimisha Urais wa Baraza Kuu

Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilitimiza mengi, yakiwemo kuafikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu na Ajenda ya Addis Ababa ya kuchukua hatua kuhusu kufadhili maendeleo.

Hayo yamesemwa na Rais wa Baraza Kuu anayeondoka Sam Kutesa, akihutubia waandishi wa habari kwa mara ya mwisho katika wadhfa huo, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

“Kipindi hiki kilitupa fursa ya kihistoria ya kuubadilisha ulimwengu wetu. Lakini juhudi zetu za kuuweka ulimwengu wetu kwenye mkondo endelevu zitafeli iwapo hatutakabiliana na moja ya changamoto muhimu zaidi katika nyakati zetu- mabadiliko ya tabianchi. Itakuwa muhimu kufikia mkataba madhubuti na kabambe mjini Paris, utakaoendeleza kufikia maendeleo endelevu, huku tukiitunza sayari dunia”

Aidha, Bwana Kutesa amepongeza jinsi Baraza Kuu lilivyoitikia changamoto mpya, kama vile mlipuko wa Ebola, ambapo lilipitisha azimio la kuanzisha ujumbe wa kushughulikia dharura ya Ebola, UNMEER, ukiwa ni wa kwanza wa aina yake.

Amegusia pia moja ya ufanisi mkubwa zaidi wakati wa muhula wake

“Katika kipindi hiki, nilifanya marekebisho ya Baraza la Usalama moja ya vipaumbele vyangu, ili kufanikisha harakati hizo. Pamoja, ni lazima tuwe na ari ya kubadilisha Baraza la Usalama ili lionyesha uhalisia wa hali kisiasa na kijiografia. Nakaribisha kupitishwa kwa azimio la pamoja la kusongesha kazi hii mbele, kwa msingi kwa kazi iliyofanyika muhula huu.”

Matukio mengine muhimu aliyoyataja ni pamoja na kuzindua muongo wa watu wenye asili ya Afrika mwezi Disemba 2014, na kutolewa kwa tuzo ya kwanza ya Nelson Rolihlahla Mandela