Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD yatoa mapendekezo ya kutokomeza umaskini

UNCTAD yatoa mapendekezo ya kutokomeza umaskini

Shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCTAD, limetoa leo ripoti yake ya mwaka kuhusu jitihada za kupambana na umaskini, likisema hadi dola trilioni 4.5 zinapaswa kuwekezwa kila mwaka katika miundombinu, uhakika wa chakula, mazingira, afya na elimu.

Akiongea na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi, Katibu Mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi amesema tayari watu bilioni moja wameepuka na umaskini uliokithiri kwa kipindi cha miaka 20.

(Sauti ya Kituyi)

“ Lakini sisi tukifurahia malengo ya maendeleo ya milenia, bado tunaamini kwamba mafanikio mengi yamefanywa lakini hayakuwa sawa. Sasa hivi ni mwaka 2015 na dunia imejipa lengo la juu zaidi.  Tunasema kwamba kwa kipindi cha miaka kumi na tano ijayo tunataka kutokomeza umaskini uliokitithiri. Ina maana tunahitaji ari kubwa kuhusu tunachopaswa kufanya ili  kutimiza malengo hayo.” 

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo, umaskini na utofauti bado ni changamoto kubwa.

Bwana Kituyi amependekeza aina nne za hatua zinazopaswa kuchukuliwa zikiwemo kubadilisha mifumo ya uchumi, kuimarisha mamlaka za serikali na masoko, kupambana na hali hatarishi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

UNCTAD inatarajia kujadili kuhusu ripoti hiyo katika mkutano wake wa mwaka utakaofanyika mwezi Machi, mwaka 2016, nchini Peru.