Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawakilishi wa mazungumzo Libya waafikia vipengele muhimu vya makubaliano

Wawakilishi wa mazungumzo Libya waafikia vipengele muhimu vya makubaliano

Wawakilishi wa baraza la kitaifa nchini Libya wameondoka mjini Skhirat, Morocco kwa kipindi cha saa 48, ili wafanyie tathmini vipengele muhimu vya rasimu ya makubaliano ya amani,  na baadaye kurejea na orodha ya majina ya wagombea wa serikali ya muungano.

Tayari, washiriki wengine katika mazungumzo hayo wamewasilisha majina ya wagombea wao, wakiwemo wawakilishi wa bunge.

Akiongea na waandishi wa habari, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Bernardino Leon, amesema ana matumaini kuwa msukumo na moyo mwema ulioonekana katika mazungumzo yaliyofanyika hadi usiku wa manane utaendelea, na kwamba rasimu ya makubaliano ya amani itaungwa mkono na kila mshiriki katika mazungumzo.

Bwana Leon amesema pande zote zimeweka maslahi ya taifa la Libya mbele, na kwamba wameonyesha utashi wa kisiasa na ukarimu ili kufikia makubaliano hayo.