Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kuondoa ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika

Harakati za kuondoa ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika

Septemba nane kila mwaka ni siku ya kuondoa ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni kujua kusoma na kuandika na jamii endelevu.

Ujuzi wa kusoma na kuandika umetajwa kama ufunguo wa maendeleo endelevu au SDGs yanayopitishwa baadaye mwezi huu yakiitwa pia ajenda 2030,  kwani ndio msingi wa stadi, mitazamo na maadili ambayo yanahitajikwa kwa ajili ya kujenga jamii endelevu.

Katika ujumbe wake kwa siku hii Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova ametoa wito kwa nchi wanachama na wadau kuongeza juhudi maradufu-kisiasa na kiufadhili katika kuhakikisha kwamba ujuzi wa kusoma na kuandika unatambuliwa kama kiuongo muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu. Kadhahlika amesema kwamba mustakhabali mwema unaanza na alfabeti yaani A BE CHE na kadhalika!

Kwa mantiki hiyo nchi zinapaswa kuzingatia umuhimu huu katika mipango yake. Je hali ikoje Afrika Mashariki? Tuanzie nchini Uganda ambako  bado asilimia 25 ya watu hawajui kusoma wala kuandika, wengi wao wakiwa ni wanawake.  Kupitia mradi wa kitaifa wa FAL, yaani mradi wa kufundisha kusoma na kuandika, ulioanzishwa na serikali tangu miaka ya 90,  watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi wanaweza kubadilisha maisha yao.

John Kibego kutoka Uganda anaeleza zaidi.

Nako nchini Tanzania takwimu zinaonyesha hali halisi kama anavyoelezea Tumsofu Mmari ambaye ni mtaalam wa masuala ya elimu kutoka UNESCO nchini humo alipohojiwa na Grace Kaneiya wa idhaa hii.