Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzuri wa Uganda waonyeshwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa

Uzuri wa Uganda waonyeshwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa

Maonyesho kuhusu Uganda yamezinduliwa jana usiku kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwa ajili ya kuvutia watalii na wafanyabiashara kwenye nchi hiyo iliyopewa jina la lulu ya Afrika.

Akiongea kwenye uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepongeza kazi zilizotekelezwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa, mwenye uraia wa Uganda, wakati ambapo anakaribia kuhitimisha mamlaka yake. Aidha Ban amezingatia umuhimu wa utalii:

“ Utalii unachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa kimataifa, na unaweza kuendeleza utunzaji wa mazingira. Zaidi ya watalii bilioni moja wamevuka mipaka ya kimataifa mwaka jana. Maonyesho haya yanatuonyesha uzuri wa mazingira na viumbe wa pori . Inatukumbusha uwajibikaji wetu wa kutunza mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Halikadhalika Waziri wa Utalii wa Uganda, Maria Mutagamba amemulika umuhimu wa utalii kwa uchumi wa Uganda akisema ushirikiano wa kikanda umewezesha Uganda kukuza fursa za utalii nchini humo.