Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha mapendekezo ya Kamisheni ya Ulaya kuhusu wakimbizi na wahamiaji

UNHCR yakaribisha mapendekezo ya Kamisheni ya Ulaya kuhusu wakimbizi na wahamiaji

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limekaribisha mapendekezo ya Kamisheni ya Muungano wa Ulaya yaliyotangazwa Jumatano wiki hii kushughulikia mzozo wa wakimbizi uliopo sasa Ulaya.

Shirika hilo limesema, kutokana na udharura wa hali iliyopo sasa hivi, mapendekezo hayo yanapaswa kutekelezwa kikamilifu na haraka.

UNHCR imesema mkakati uliopendekezwa wa kuwahamisha wakimbizi 160,000 kutoka Ugiriki, Italia na Hungary, utasaidia kwa kiwango kikubwa kukabiliana na mzozo huo. William Spindler ni msemaji wa UNHCR, Geneva

Makadirio yetu ya awali yanaonyesha mahitaji makubwa hata zaidi, lakini la kuzingatia sasa ni kuhakikisha kuwa nchi zote wanachama wa EU zinashiriki mkakati huu, na kwamba unatekelezwa haraka. Wakati wakihamishwa, mahitaji ya wakimbizi na mapendeleo yao na hali zao halisi zinapaswa kuzingatiwa kadri iwezekanavyo.”

UNHCR imesema mkakati huo wa kuwahamisha wakimbizi utafaulu tu iwapo utaambatana na mapokezi makubwa ya dharura, usaidizi na usajili katika nchi zinazoathiriwa zaidi na wakimbizi wanaowasili Ulaya, mathalan Ugiriki, Hungary na Italia.