Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio lapitishwa kupeperusha bendera za Palestina na Holy See Umoja wa Mataifa

Azimio lapitishwa kupeperusha bendera za Palestina na Holy See Umoja wa Mataifa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kuruhusu kupeperushwa kwa bendera za Palestina na Holy See kwenye makao makuu jijini New York, Marekani na katika ofisi zake kwingineko.

Kabla ya kupiga kura, mwakilishi wa Iraq ambayo ni kiongozi wa nchi za kiarabu kwa mwezi huu wa Septemba alitoa maelezo ya azimio hilo namba A/69/L.87 kuhusu kuimarisha mfumo wa Umoja wa Mataifa lilijikita zaidi katika hoja ya kupeperusha bendera za wanachama wa Umoja huo wasio na hadhi ya utazamaji kwenye chombo hicho ambao ni Palestina na Holy See.

Alieleza kuwa azimio linapendekeza bendera hizo kupepereshwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na ofisi zake pindi bendera hizo zitakapowasilishwa na wanachama hao.

Halikadhalika linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa achukue hatua stahiki kwa utekelezaji wakati wa mkutano wa 70 wa Baraza Kuu na ndani ya siku 20 baada ya azimio hilo kupitishwa.

Hatimaye wakati wa upigaji kura uliwadia na ulifanyika kielektroniki ili kutunza kumbukumbu

Muongozaji anasema kuwa Baraza Kuu sasa linapigia kura azimio namba A/69/L.87/Rev 1 liitwalo kupeperusha bendera za wanachama wasio na hadhi ya utazamaji…….upigaji kura umekamilika tafadhali funga mashine……

Na hatimaye matokeo..

Anasema waliounga mkono 119, waliopinga Wanane , wasioonyesha msimamo wowote 45.

Miongoni mwa nchi zilizopinga ni Marekani na Israel, ambapo mwakilishi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour akazungumza baada ya tukio hilo.

(Sauti  ya Mansour)

“Tunatoa shukrani kwa nchi wanachama waliounga mkono azimio hili. Kura ya nchi wanachama leo ni thibitisho la msimamo wa muda mrefu wa jamii ya kimataifa wa kuunga mkono suluhu la kina la haki, la kudumu na la amani, kwa suala la Palestina, na kuunga mkono utimizaji wa haki ya msingi ya watu wa Palestina, ikiwemo madaraka yao na uhuru.”

Miongoni mwa nchi wa Afrika zilizounga mkono uwasilishaji wa azimio  hilo ni Namibia, Zimbabwe, Sierra Leone na Afrika Kusini.