Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 30 ya shule nchini CAR zimeshabuliwa: ripoti

Asilimia 30 ya shule nchini CAR zimeshabuliwa: ripoti

Mtandao wa kijamii wa Watchlist umezindua leo ripoti kuhusu mashambulizi dhidi ya shule nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ukisema karibu asilimia 30 ya shule 335 zilizochunguzwa zimeshambuliwa kati ya mwaka 2012 na mwezi Aprili 2015. Aidha asilimia 8 ya shule hizo zimetumiwa na vikundi vya waasi au walinda amani.

Watchlist imesikitishwa pia na kuona kwamba mpaka sasa hivi asilimia 65 ya shule nchini kote zimefungwa, ikiiomba serikali ya mpito pamoja na jamii ya kimataifa ichukue hatua ya kuimarisha usalama wa mazingira ya shule nchini humo.

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini New York, Marekani, mtafiti kutoka shirika la Watchlist Janine Morna, amesema mara nyingi shule zinaporwa, na wanafunzi na walimu wanatishiwa.

“ Waasi wakiingia kwenye kijiji, wanakalia eneo la shule na wanapora vifaa vyake. Wanaiba milango ya shule, meza, viti, vitabu ambavyo hugeuza kuni. Aidha wameuza vifaa vyenye thamani kama mabati na vifaa vingine kwa faida yao.”