Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa dola milioni 250 utawezesha watoto milioni 1 wa Syria kwenda shule- Brown

Mchango wa dola milioni 250 utawezesha watoto milioni 1 wa Syria kwenda shule- Brown

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Duniani, Gordon Brown, amesema ingawa ulimwengu sasa unamulika wakimbizi wanaoingia barani Ulaya, kuna wakimbizi wa Syria milioni nne  walioko katika nchi za Jordan, Uturuki na Lebanon, milioni mbili miongoni mwao wakiwa watoto.

Akiongea na wanahabari mjini New York kwa njia ya simu, Bwana Brown amesema mzozo wa wakimbizi wa Syria una madhara makubwa kwa watoto, na kuna haja ya kuchukua hatua za dharura.

Kwa mantiki hiyo, ametangaza mapendekezo kadhaa ya  hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika siku 21 zijazo, ili kukabiliana na baadhi ya matatizo yanayowakabili hususan watoto wa umri wa kwenda shule.

Mfano wa mapendekezo hayo ni kugawa madarasa na masomo katika sehemu mbili, ambapo nchini Lebanon, watoto wa Lebanon watafundishwa katika lugha za Kiingereza na Kifaransa asubuhi na mchana, na watoto wa Syria kufundishwa katika lugha ya Kiarabu kwa saa zilizosalia kila siku.

Licha ya hayo, Bwana Brown amesema tatizo  nchini Lebanon, kama ilivyo Uturuki na Jordan, si ukosefu wa walimu au madarasa, bali ni uhaba wa fedha

“Tunaamini kuwa ufadhili wa milioni 250 zaidi kutoka jamii ya kimataifa, tunaweza kuwapeleka watoto milioni moja shuleni. Kwa kawaida, elimu hutelekezwa kwa sababu usaidizi wa kibinadamu huenda kwa chakula na makazi, na misaada ya maendeleo huwa haipangiwi dharura. Lakini tuna mapendekezo hapa yanayoweza kuwapeleka watoto milioni shule.”