Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naondoka DR Congo nikiwa na matumaini makubwa: Kobler

Naondoka DR Congo nikiwa na matumaini makubwa: Kobler

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Martin Kobler, amesema amehitimisha jukumu lake kwa mafanikio makubwa ikiwemo kutokomeza kikundi cha M23, na yote ni kutokana na ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wote. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kobler ambaye aliteuliwa mwezi Juni mwaka 2013 kuwa mwakilishi wa Katibu mkuu na Mkuu wa ujumbe wa umoja wa Mataifa, DR Congo, MONUSCO amesema hayo mjini Goma alipozungumza na wafanyakazi akieleza kuwa wakati ulikuwa mgumu hasa kampeni ya kutokomeza waasi wa M23 mwezi Novemba  mwaka 2013.

Kobler amesema awali wananchi walikuwa na wasiwasi hata kumrushia mawe lakini sasa wameona matunda ya kazi iliyofanywa na hata anasikia uchungu kuondoka lakini hana budi kufanya hivyo.

(Sauti ya Kobler)

“Naondoka nikiwa nimeridhika kwa kuwa tumefanikiwa mengi, lakini bado kuna mengi ya kufanywa na atayechukua nafasi hii. Kuna suala la waasi wa FDLR ambalo bado limekwama, siyo tatizo la majenerali wawili kwa kuwa hilo tayari limetatuliwa lakini kwa kweli tunapaswa kushughulikiwa tatizo la FDLR.”

Amerejelea wito wake kuwa iko siku MONUSCO itaondoka DRC lakini katika mazingira ambayo kwayo amani iliyokwishapatikana haitatumbukia nyongo bali itadumu kwa mustakbali bora wa wananchi.