Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokidhi mahitaji ya kibinadamu Syria kunaongeza mzozo wa watoto wakimbizi- UNICEF

Kutokidhi mahitaji ya kibinadamu Syria kunaongeza mzozo wa watoto wakimbizi- UNICEF

Mzozo wa wakimbizi na wahamiaji Ulaya utazidi kuzorota iwapo juhudi zaidi hazitafanywa kuumaliza mgogoro wa Syria na kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya mamilioni ya watu walioathiriwa na machafuko, limesema Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

UNICEF imesema kuwa mgogoro wa Syria umewaacha watu wapatao milioni 16 wakihitaji usaidizi wa kuokoa maisha na ulinzi, huduma za afya, maji safi na elimu, na kwamba nusu ya watu hao ni watoto. Licha ya changamoto hizo, ufadhili wa usaidizi wa kibinadamu ni haba.

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wapatao milioni mbili ndani ya Syria hawaendi shule, huku angalau watu milioni tano katika miji na jamii kote nchini wakiwa wamekumbana na madhara ya kukatizwa huduma za maji katika miezi michache iliyopita.

Zaidi ya Wasyria milioni nne wamekimbilia nchi jirani na kwingineko tangu mzozo ulipoanza takribani miaka mitano iliyopita, na nusu ya wakimbizi hao ni watoto.