Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukoma wazidi kutesa nchi sita za Asia ikiwemo India na Bangladesh: WHO

Ukoma wazidi kutesa nchi sita za Asia ikiwemo India na Bangladesh: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetaka kuimarishwa kwa jitihada za kutokomeza magonjwa ya kitropiki yasiyopatiwa kipaumbele kama vile ukoma, mabusha, matende na kichocho ambayo yanaendelea kulemaza, kutesa na kuua watu huko Kusini Mashariki mwa Asia.

Mkurugenzi wa WHO kwenye ukanda huo Dokta Poonam Khetrapal Singh amesema magonjwa hayo yanayotibika, yanakumba pia watu wasiopatiwa kipaumbele ambao ni mafukara na hivyo amesema ahadi mpya thabiti za kisiasa zinatakiwa kutokomeza magonjwa hayo.

Akizungumza kwenye mkutano wa mawaziri wa afya na maafisa wa andamizi kutoka nchi 11 huko Dili, Timor-Leste, amesema waathirika husalia pia na unyanyapaa kutoka kwa jamii iliyowazunguka na hatimaye kutumbikia kwenye umaskini.

India, Bangladesh, Indonesia, Myanmar, Nepal na Sri Lanka zimetajwa kuongoza duniani kwa kuwa na visa vingi zaidi za Ukoma ambako kila mwaka kuna visa vipya 1000 na mwaka 2013 asilimia 60 ya wagonjwa wote wa ukoma duniani walikuwepo eneo hilo.