Matumizi holela ya viua vijasumu yaathiri afya ya umma:WHO
Shirika la Afya Duniani WHO limesema kwamba matumizi holela ya viua vijasumu au Antibiotics, na madawa mengine yanasababisha usugu kwa madawa hayo na watu kushindwa kupona.
Mkurugenzi wa WHO kwa Ukanda wa Asia Kusini Mashariki, Daktari Poonam Khetrapal Singh amesema hayo akihutubia mkutano wa kikanda unaofanyika nchini Timor-Leste, akieleza kwamba hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kupambana na nguvu kinzani ya binadamu dhidi ya viua vijasumu ambayo ni hatari kubwa kwa afya ya umma.
Ameonya kwamba iwapo hatua hazitachukuliwa, magonjwa ambayo sasa yanatibiwa na viua vijasumu huenda yakaua mamilioni ya watu.
Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WHO imeeleza kwamba nguvu kinzani hiyo imesababishwa na matumizi mabaya ya madawa, watu kutomaliza matibabu yao mpaka mwisho, wakulima kulisha mifugo viua vijasumu na usafi duni hospitalini.