Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa 4 vipya vya homa ya matumbo vyapatikana Yarmouk

Visa 4 vipya vya homa ya matumbo vyapatikana Yarmouk

Wahudumu wa afya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA wameweka kituo cha afya kwenye mtaa wa Yalda nchini Syria, ambako wamewatibu wagonjwa 280 kwa siku moja. Miongoni mwa wagonjwa hao walikuwamo wanne walioambukizwa homa ya matumbo.

UNRWA pia imetowa tembe 200,000 za kutakatisha maji zilizotolewa na UNICEF kwa jamii ya Yalda.

Wakati hali ya joto la msimu wa kiangazi na uhaba wa maji safi na chakula vikiendelea kuathiri Yarmouk, Yalda, Babila na Beit Saham, magonjwa ya kuambukiza yanasalia kuwa tishio kubwa kwa raia.

Huduma za afya katika maeneo hayo ni haba, na uwezo wa kukabiliana na milipuko mikubwa na mahitaji mengine makubwa ya kiafya haupo.