Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvumbuzi unaojali mazingira watunukiwa kwenye tuzo za SEED

Uvumbuzi unaojali mazingira watunukiwa kwenye tuzo za SEED

Wakati ulimwengu ukijiandaa kuridhia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) mwishoni mwa mwezi huu, kampuni 27 zinazoongoza katika uvumbuzi unaojali mazingira na kufaidi jamii zimetunukiwa kwenye kongamano la Afrika la SEED, mwaka 2015, ambalo linafanyika jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, tuzo za SEED hutambua ujasiriamali bunifu wa kijamii na mazingira, ambao biashara yake husaidia kukabiliana na changamoto za maendeleo endelevu.

Tuzo za mwaka 2015 zimemulika bara Afrika, 25 zikinyakuliwa na kampuni kutoka Ethiopia, Kenya, Malawi, Musumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda. Tuzo nyingine mbili zimetunukiwa kwa biashara zinazoongozwa na wanawake, kama njia ya kuendeleza usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake.