Jamii ya kimataifa isaidie ulinzi wa urithi wa kitamaduni: Eliasson
Mkutano wa kimataifa kuhusu harakati za ulinzi wa mali za urithi wa kitamaduni na mateso dhidi ya jamii za kidini unaendelea huko Paris, Ufaransa, ambapo awali Naibu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema juhudi za kimataifa zinahitajika ili kuepusha vitendo hivyo.
Akizungumza mjini humo kabla ya kuanza kwa mkutano huo unaohudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Bwana Eliasson amesema dunia inapaswa kushirikiana kukabilia vitisho dhidi ya mali za urithi wa kitamaduni ambazo zinakabiliwa na uharibifu kutoka vikundi vilivyojihami huko Iraq na Syria.
"Kuna wajibu mkubwa kwa wanachama wa baraza la usalama kushughulikia tatizo hili na pia kuna wajibu mkubwa kwa nchi katika eneo husika kufanya kile wanachoweza kumaliza janga hili. Hatua hiyo italeta matunda mema natumai kwa wananchi wa Syria na Iraq, halikadhalika kwa nchi jirani ambazo sasa zina shinikizo kubwa la wakimbizi, halikadhalika kwa Ulaya na nchi zingine zilizoathiriwa na vita hivi.”
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano na Ufaransa na Jordan wakati huu ambapo UNESCO inasema urithi wa kitamaduni huko Mashariki ya Kati pamoja na tofauti za kitamaduni ni lazima zihifadhiwe kwa amani ya baadaye kama sehemu ya utambulisho wa binadamu.