Skip to main content

Watu 8,000 wameuawa mashariki mwa Ukraine- ripoti ya UM

Watu 8,000 wameuawa mashariki mwa Ukraine- ripoti ya UM

Takriban watu 8,000 wameuawa mashariki mwa Ukraine tangu kati kati mwa mwezi Aprili mwaka 2014. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kumi na moja ya Umoja wa Mataifa ya ujumbe wa uangalizi wa haki za binadamu nchini Ukraine, ambayo imetolewa leo na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein.

Kamishna Zeid amesema mashambulizi ya maeneo ya makazi kutoka pande zote kinzani yamesababisha ongezeko la wahanga wa kiraia katika miezi mitatu iliyopita kwa viwango vya kutia hofu.

Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kuwalinda raia na kuumaliza uhasama, kulingana na makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Februari.

Ripoti hiyo ambayo ni ya kipindi cha kuanzia Mei 16 hadi Agosti 15 2015, inaonyesha kuwa idadi ya wahanga wa kiraia iliongezeka zaidi ya maradufu ikilinganishwa na miezi mitatu ya awali, watu 105 wakiwa wameuawa, 308 kujeruhiwa, ikilinganishwa na 60 waliouawa awali na 102 kujeruhiwa.