Skip to main content

Baraza Kuu lafanya mkutano kuhusu wajibu wa kulinda raia

Baraza Kuu lafanya mkutano kuhusu wajibu wa kulinda raia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi wanachama, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenda hatua zaidi ya kuelewa wajibu wa kulinda na kuchukua hatua za kulinda raia. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Bwana Ban amesema hayo akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo leo limekuwa na mkutano kuhusu utekelezaji wa ahadi ya wajibu wa kulinda, ambayo iliafikiwa na nchi wanachama miaka kumi iliyopita.

“Baraza la Usalama ndilo pekee lenye mamlaka chini ya sheria ya kimataifa ya kuamuru hatua za kijeshi kunusuru maisha pale hatua nyingine zote zinapofeli. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuchukua hatua mapema, kuzuia uhalifu wa mauaji na kuzisaidia nchi kuwalinda raia wao. Swali linalopaswa kuiongoza kazi ya Baraza la Usalama ni: je, kweli tumefanya kila tuwezalo?”

Ban amesema zinajua kuwa wajibu wa kuzuia na kukabiliana na uhalifu wa maangamizi ni moja ya wajibu wao wa msingi chini ya sheria ya kimataifa. Kwa mantiki hiyo, ameongeza kwamba viongozi hawawezi tena kudai kuwa uhuru wa nchi zao una uzito mkubwa kuliko kitu kingine chochote, au kusingizia hali ya taifa na matishio ya kiusalama.