Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi Arabia, Iran, Marekani na Urusi ni suluhu kwa mzozo wa Syria: de Mistura

Saudi Arabia, Iran, Marekani na Urusi ni suluhu kwa mzozo wa Syria: de Mistura

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesema iwapo kungalikuwepo na majadiliano ya dhati baina ya pande zenye ushawishi na kile kinachoendelea nchini Syria, mzozo huo ungalikuwa tayari umebakia historia, lakini kinachofanyika sasa si mambo ya dhat na ndio kinachochoea wananchi kukimbia nchi yao kwenda Ulaya.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Brussels, Ubelgiji, de Mistura amesema dana dana za mazungumzo zinaendelea na wananchi hawaoni matumaini yoyote na ndio maana wanaamua kukimbiza uhai wao na ujumbe mahsusi ni kutoka kwa mtoto Aylan aliyefariki dunia akiwa njia kuelekea Ulaya.

(Sauti ya de mistura)

“Fikira kungalikuwapo majadiliano ya dhati kati ya Urusi na Marekani! Wanakutana mara kwa mara lakini hakuna matokeo ya dhati kuhusu mzizi wa kinachoendelea Syria na mustakhbali wake. Na pili iwapo Saudi Arabia na Iran hatimaye wangalianza mazungumzo. Iwapo mashauriano hayo yangalikuwepo na ihakikishiwe hawako peke yao kwenye meza ya mazungumzo, mzozo ungalidumu mwezi mmoja tu na siyo mwaka hata miaka kumi, kwa sababu kichocheo cha mzozo kitatoweka.”

Amesema miaka mitano ndani ya mzozo wa Syria, hakuna tena muda wa mikutano na majadiliano ya muda mrefu huu ni wakati wa kutazama macho ya wasyria wanaosema hawana tena matumaini na hawawezi tena kusubiri.